Mfuko wa Barabara (Road Fund) umetoa zaidi ya Tsh mil 408.9 kwa ajili ya matengenezo ya barabara,vivuko na kalvati wilayani Kilindi
Fedha hizo zimesaidia kufanikisha matengenezo ya miundombinu ya barabara katika vijiji vya Kwediboma, Makasini,Mzinga,Kimembe,Kilwa,Majengo,Kwadundwa,Muungano na Kwadudu.
Kaimu meneja wa TARURA Wilayani Kilindi ndugu Gwamaka Mwaipaja amezitaja barabara hizo kuwa ni Kwediboma-Kimembe kilomita 9.5,Muungano-Kimembe-Tamota-Vyadigwa kilomita 3.2 na Tamota-Kwadundwa-Lulago-Lwande kilomita 2.6.
Amesema matengenezo ya barabara hizo yamehusisha ujenzi wa kalvati 6 na vivuko mfuto (solid drift) 8 na kwamba mradi huu ambao mkataba wake ulianza 03/09/2021 na kutakiwa kukamilika 03/03/2022 uliongezewa muda hadi tarehe 20/04/2022 hivi sasa umekamilika.
Bwana Mwaipaja amesema katika mradi huu matengenezo ya barabara ya muda maalum na sehemu korofi yalikuwa barabara ya Kwediboma-Kimembe,ambapo matengenezo ya muda maalum yalihusisha barabara ya Tamota-Kwadundwa-Lulago-Lwande na matengenezo ya kawaida yalihusisha barabara ya Muungano-Kimembe-Tamota-Vyadigwa.
Amesema TARURA wilayani Kilindi kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji husika inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza barabara pamoja na kuacha shughuli zote zinazosababisha uharibu wa miundombinu hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilindi ndugu Gracian Makota akizungumzia kuhusu matengenezo ya barabara hizo amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania Mh: Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitatua changamoto ya ubovu wa barabara kwa kutoa fedha.
Amewataka wafugaji kuacha kupitisha mifugo katika barabara kwani tabia hiyo imekuwa ikiharibu miundombinu hiyo.
Amewataka watendaji wa kata na vijiji kushirikiana na TARURA kuelimisha wananchi kuacha kulima au kufanya vitendo vyovyote vinavyosababisha uharibu wa barabara na mindombinu mingine.
Matengenezo ya barabara hizi yatasaidia wakazi wa maeneo ya Lwande,Kwadundwa,Tamota,kupitisha mazao yao kwa urahisi kwani maeneo haya ni tajiri wa mazao ya viungo kama vile Iliki,Mdalasini,Pilipilimanga,Ndizi,Magimbi na mengine mengi.
MODI MNGUMI
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.