Mkuu wa Wilaya Kilindi Mh:Abel Yeji Busalama amesema suala la kuweka mifugo Hereni ni endelevu na kila mfugaji wilayani hapa anatakiwa kutekeleza agizo hilo.
Mh:Mkuu wa Wilaya ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati alipokuwa akizungumza na wafugaji wilayani Kilindi katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi.
Amesema kila mfugaji anatakiwa kuweka Hereni Mifugo yake na asiyefanya hivyo hatua za kukamatwa mifugo yake itachukuliwa
“Kila mfugaji katika kila kata kwa viongozi wa wafugaji na wafugaji maarufu muwe wa kwanza kuweka hereni ili wengine waweke kama ulihamisha Ngombe wako kwa sababu ya kiangazi basi watakapokuja tena utatoa taarifa” alisistiza Mh:Busalama
Amesema zoezi la kuweka hereni ni endelevu kwa sababu kila siku mifugo inazaliwa na kuongezeka hivyo kila mfugaji anapaswa kutekeleza agizo hilo ili kuepuka kamatakamata hapo baadaye.
Akizungumzia kuhusu vifo vya mifugo Mh:Busalama amewataka wafugaji kutoa taarifa mara moja kunapotokea vifo vya mifugo katika maeneo yao.
Amesema suala la vifo vya mifugo kufa na sababu haijulikani ni sehemu ya majukumu ya kamati ya usalama wilaya na wasing’ang’anie kutibu wakati kuna kitu hakijulikani inapaswa kutafutwa chanzo cha tatizo.
Katika kikao hicho wafugaji wengi waliomba serikali kusitisha zoezi la uwekaji hereni mifugo yao kwa madai kuwa hivi sasa kwa sababu ya kiangazi mifugo mingi haipo karibu imepelekwa mbali kwa ajili ya malishona kuongeza kuwa serikali ingesubiri hadi wakati wa mvua ndipo zoezi hilo lianze
Wafugaji hao katika kikao hicho pia walipendekeza kuwepo kwa maeneo maalum ya wafugaji ambayo yatatambuliwa kisheria kwa wafugaji kumilikishwa maeneo hayo baada ya kufuata taratibu zote za kisheria.
Wamesema maeneo hayo yanapaswa kutambuliwa kisheria na wafugaji kwa kushirikiana na wataalam wa kilimo na mifugo kuanzisha mashamba ya malisho kwa ajili ya mifugo yao hali ambayo inaweza kuondoa migogoro ya ardhi kati yao na wakulima
Modi Mngumi.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.