Mkuu wa wilaya Kilindi Mhe. Hashim Mgandilwa amewataka wakazi wa Kijiji Cha Mgera waliojenga kando kando ya mto Lukigula kuhama makazi hayo ili kunusuru maisha yao kufuatia maporomoko ya udongo yanayoendelea kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Mh. Mgandilwa aliyasema hayo Disemba,16 alipofanya ziara katika Kijiji hicho akiambatana na kamati ya Usalama wilaya kwa lengo la kujionea uharibifu wa daraja la Mgera uliotokana na mvua kubwa na kusababisha kusombwa na maji na kukatisha mawalisiano baina ya vitongoji viwili vilivyopo ndani ya Kijiji hicho.
Madhara ya kutokuwepo kwa kivuko hicho kunaathiri upatikanaji wa huduma zote za kijamii ambazo zipo ng'ambo ya pili ya mto huo zikiwemo zahanati, shule na ofisi ya Tarafa.
Akihutubia wananchi mbele ya mkutano wa hadhara ameitaka Mamlaka husika ya usimamizi wa barabara za vijijini Tarura Mkoa wa Tanga na Wilaya kuchukua hatua za haraka za kurejesha miundo mbinu kwa muda ili kuwezesha wananchi kuvuka kwa uhakika na kupata huduma za msingi zilizopo ng'ambo ya mto huo.
Mwisho aliwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati Serikali inaendelea kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto hiyo .
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.