Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa Kata ya Bokwa Mhe. Idrissa Omari Mgaza, imekagua miradi ya elimu kwa lengo la kujiridhisha na hatua za ujenzi zilizofikiwa ili iweze kutoa huduma bora kwa jamii.
Akiwa katika ziara hiyo iliyohusisha wakuu wa idara na vitengo pamoja na waheshimiwa Madiwani, Mhe.Idrissa Omari Mgaza alipata fursa ya kuona, kukagua, kusikiliza na kuainisha hatua zilizofikiwa, fedha iliyotumika na iliyobakia, ubora na changamoto zilizopo katika miradi hiyo ili ziweze kutatuliwa kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Amesema sekta ya elimu ni sekta muhimu sana na ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya sasa na ya baadae hivyo ni vema kuweka mkakati madhubuti wa ufuatiliaji kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora uliokusudiwa.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa miradi yenye ubora hupelekea kutoa huduma bora kwa wananchi kutakakoimarisha ubora wa elimu inayotolewa na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi hali itakayoleta hamasa kwa walimu katika ufundishaji, wanafunzi katika kujifunza na mwamko wa kusomesha watoto katika jamii.
"Sekta ya Elimu ni sekta inayomgusa mwananchi moja kwa moja, hivyo nilazima tujiridhishe miradi hii inatekelezwa kwa viwango na thamani ya fedha inaonekana ili iweze kutoa huduma bora kwa jamii" Amesisitiza Mhe.Idrisa
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni pamoja na ujenzi wa darasa, ofisi na stoo shule ya msingi Songe, Maabara katika shule ya sekondari Seuta katika kata ya Songe, ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya msingi Nkama, ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo katika shule ya sekondari Nkama katika kata ya Bokwa.
Imeandaliwa na
Kitengo Cha TEHAMA
Halmashauri ya Kilindi.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.