Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mheshimiwa Sauda Mtondoo amewataka viongozi waliochaguliwa wa Serikali za vijiji na Vitongoji kutokuanzisha migogoro katika maeneo yao badala yake wakatatue Migogoro katika Maeneo yao ya Utawala.
Mhe. Mtondoo ameyasema hayo alipokuwa akifungua Semina maalumu kwa Viongozi waliochaguliwa Mwaka 2019 iliyoambatana na zoezi la kuwaapisha Viongozi waliochaguliwa kuongoza Serikali za Vijiji na Vitongoji.
“Hatuta mfumbia macho kiongozi atakaye kuwa chanzo cha Migogoro katika maeneo yenu” alisema Mkuu wa Mtondoo katika Mafunzo hayo. Aidha aliwataka Viongozi hao kutunza na kuenenda sawa na Viapo vyao ili kuondokana na Migogoro katika maeneo yao.
Mafunzo haya ya siku tano (05) yameanzishwa ili kuwajengea uwezo viongozi kabla ya kuanza kazi yakiwa na lengo la kutatua na kupunguza migogoro ambayo imekuwa ni tatizo sugu kwa Serikali za Vijiji na Vitongoji.
Wawezeshaji katika mafunzo haya ni kutoka Idara ya Utumishi, Mipango, Ugavi , Maendeleo ya Jamii, Ardhi, Sheria na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.
Aidha Afisa Utumishi Wilaya Ndg. Edward Masona amewataka Viongozi hao kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu za kiongozi lakini pia wanafanya Mikutano ya Vijiji na kusoma taarifa ya Mapato na Matumizi kila baada ya miezi mitatu ili kuondokana na Migogoro isiyokuwa ya lazima.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Ndg. Geofrey Msuya amewahimiza viongozi kushirikisha jamii katika Mipango mbalimbali ya maendeleo badala ya kufanya maamuzi kama viongozi bila jamii kushirikishwa hali inayopelekea wananchi kutoshiriki katika Miradi ya Maendeleo. Lakini pia amewataka Viongozi kuwa Mfano katika Jamii kwa kuonyesha njia kwa jamii zao.
Imetolewa na:
Samwel Daniel Mwantona
Afisa TEHAMA
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.