Watendaji wa kata na vijiji watakiwa kuhakikisha wanasimamia upandaji miti katika maeneo yao ili kuweza kuhimili mabadiliko ya tabia ya nchi na mifumo ya hali ya hewa inayopelekea kupata mvua chini ya kiwango na nyakati ambazo hazikutarajiwa.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda S.Mtondoo alipokuwa akizindua wiki ya upandaji miti katika Shule ya Sekondari Nkama iliyopo kata ya Bokwa wilayani hapa. Ambapo katika sherehe hizo watendaji mbalimbali wa serikali walishiriki.
Hata hivyo Mhe. Mtondoo amewataka watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanaandaa utaratibu wa kupanda miti katika maeneo ya kaya, Ofisi za serikali za vijiji, Vituo vya Afya, Shule za msingi na Sekondari lakini pia katika miteremko ya milima na maeneo yote ya wazi.
“Maafisa watendaji wa vijiji kaanzisheni sheria ndogo zitakazo sisitiza upandaji miti kwa wananchi” alisema Mkuu wa wilaya alipokuwa akitoa maagizo kwa watendaji na kueleza umuhimu wa upandaji miti katika maeneo ya makazi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi Ndg. Clemence A.Mwakasendo amesema kuwa Halmashauri kupitia idara ya Ardhi na Mali Asili imejipanga kuhakikisha kuwa kata zote 21 zinatengeneza vitalu vya miche ya miti na kushiriki kwenye kampeni za upandaji miti kila mwaka.
Ndg Mwakasendo ameahidi kupitia idara ya Ardhi na Mali Asili ataendelea kushirikiana na wananchi wa Kilindi kwa kuwapatia elimu kwa kutumia maafisa ugani waliopo katika ngazi za kata na vijiji ili kutimiza adhima ya Tanzania ya kijani.
Hata hivyo wilaya ya kilindi imekuwa ikitekeleza upandaji Miti kwa vitendo kila mwaka, ambapo mwaka 2016/2017 ilijiwekea lengo la kupanda miti milioni moja laki tisa na sabini na tatu elfu na walifanikiwa kuipanda na kati ya hiyo miti milioni moja laki nane na ishirini na tano elfu sawa na asilimia 92.4 ilikua bila shida.
Kilele cha maadhimisho hayo kinatarajiwa kufanyika katika shule ya sekondari Mkindi mnamo tarehe 13 April 2018 kuanzia majira ya saa 3:00 asubuhi ambapo wananchi wote wamekaribishwa kushiriki kilele hicho.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.