Wakazi wa Wilaya Kilindi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ili kuwezesha kupatikana Takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kwa usahihi
Wito huo umetolewa leo na Mh:Abel Yeji Busalama ambaye ni Mkuu wa wilaya Kilindi katika viwanja vya shule ya sekondari ya Seuta iliyopo katika kata ya Songe, wakati wa maandamano ya kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 wilayani Kilindi.
Alisema kupitia Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 wakazi wa Wilaya Kilindi wataweza kupat mgao wa fursa za kimaendelo kulingana na idadi ya watu wake na hivyo kuwezesha jamii kunufaika na hatimaye kupata maendeleo stahiki
Alisema Taifa la Tanzania lilifanya Sensa mwaka 2012 na tangu kipindi hicho Wilaya Kilindi imepitia mabadiliko mbalimbali ikiwemo ongezeko la wageni kutoka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kama vile waliohamia kutoka mkoa wa Arusha pamoja na wageni kutoka nje ya nchi wanaofanya shughuli mbalimbali kama za migodini.
Mh:Busalama alisema kufuatia ongezeko hili hata mahitaji ya huduma za kijamii yameongezeka,hivyo Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 itatoa taswira halisi ya idadi ya watu na mahitaji yao na mambo mengine mengi ya kimaendeleo na kuwezesha serikali na wadau wake wa maendeleo kupanga mipango ya maendeleo kulingana na mahitaji ya watu waliopo.
“Takwimu za watu na nyinginezo zitakazopatikana katika zoezi la Sensa zitawezesha Mh:Mbunge,Wah:Madiwani na wadau wengine kujenga hoja za migao ya fursa za maendelo kwa mujibu wa Takwimu sahihi”Alisema Mh:Busalama na kusisitiza wakazi Wilayani hapa kuhamasishana kushiriki zoezi la Sensa kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Alisema hakuna haja ya kuficha jambo wakati kaya itakapotakiwa kutoa taarifa zake kwa karani wa Sensa kwani taarifa zote ni siri na Sensa haihitaji jina wala dini ya mtu,hitaji la Sensa ni Takwimu na taarifa mbalimbali za kimaendeleo ambazo zitaulizwa wakati wa zoezi na kuwataka wakuu wa kaya kutowaficha walemavu,wazee na hata wagonjwa wa akili kwani nao ni sehemu ya jamii na wana mahitaji yao ya msingi yanayopaswa kuwekwa katika mipango ya maendeleo.
Akizungumza katika uhamasishaji huo Mbunge wa Jimbo la Kilindi Mh:Omary Kigua alisema Sensa ni muhimu katika Taifa lolote duniani, ndiyo maana serikali ya Tanzania ilitenga zaidi ya Tsh Bilioni 370 kwa ajili ya zoezi hili muhimu na kwamba hakuna nchi yeyote inayoweza kupanga mipango ya maendeleo bila kuwa na Takwimu sahihi za wananchi wake na mahitaji yao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi Mh:Idrisa Mgaza akizungumzia Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 alisema mkazi yeyote wa Wilaya Kilindi anatakiwa kuhesabiwa na yeyote ambaye hatahesabiwa atakuwa hajaitendea haki na itakuwa sawa na mtu aliyeidhulumu Wilaya kwa kuikosesha kupatikana takwimu sahihi.
Akizungumzia maandalizi Mratibu wa Sensa Wilaya Kilindi Thadeus Kway alisema kila kitu kipo tayari kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 itakayofanyika katika Wilaya Kilindi ambayo ina kata 21,vijiji 102 na vitongoji 608 na kuwataka wakazi wilayani hapa kushiriki na kuhakikisha kila mtu katika kaya anahesabiwa.
Baadhi ya Viongozi wengine walioshiriki maandamano ya kuhamasisha Sensa yaliyoongozwa na Mh:Mkuu wa Wilaya Kilindi ni Katibu Tawala Wilaya,Katibu wa CCM Wilaya,Mkurugenzi Mtendaji na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi na wananchi mbalimbali.
NA: MODI MNGUMI
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.