KILINDI WAADHIMISHA SIKU YA KUZALIWA YA RAIS SAMIA KWA UPANDAJI MITI
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilindi, Mkoa wa Tanga, kwa kushirikiana na walimu na wanafunzi wa shule za msingi na chuocha VETA wamefanya zoezi la upandaji miti katika shule mbalimbali wilayani humo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mhifadhi Mwandamizi wa TFS Wilaya ya Kilindi, Bw. Jaspeace Kabobo, amesema zoezi la upandaji miti ni sehemu ya kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kulinda mazingira pamoja na kuendeleza kampeni ya kitaifa ya uhifadhi wa misitu. Aidha, alieleza kuwa miti iliyopandwa Januari 27 mwaka jana katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Kilindi imeendelea kukua vizuri na inaonesha matokeo chanya, jambo linalothibitisha umuhimu wa kuendeleza juhudi za upandaji na utunzaji wa miti.
Kwa upande wao, walimu na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Kilindi wameeleza kuwa miti hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, kutoa hewa safi pamoja na kuchangia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Wilaya ya Kilindi imepanga kupanda zaidi ya miti laki moja (100,000) kwa mwaka huu wa 2026. Hadi sasa, jumla ya miti 36,000 tayari imeshatolewa na kupandwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo.
Katika zoezi hilo, Kamera ya Halmashauri ilishuhudia walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Baraka wakishiriki kikamilifu zoezi la upandaji miti, huku wakitoa pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa pamoja na kuendelea kuhamasisha Watanzania kushiriki katika utunzaji wa mazingira.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.