Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 Mhandisi Charles F.Kabeho amewataka wakazi wa Wilaya Kilindi kujenga utamaduni wa kuwekeza katika elimu kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza wakati akitoa ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 katika wilaya Kilindi kijiji cha Mkindi Mhandisi Kabeho alisema jamii ina wajibu wa kuwekeza katika elimu kwa kujenga miundombinu ikiwemo madarasa,vyoo na miundo mingine kwa ajili ya kuweka mazingira bora yatakayosaidia watoto kusoma vizuri.
Wananchi wa Kata ya Mkindi waliokusanyika kuupokea mwenge wa Uhuru ndani ya kijiji cha Mkindi, Wakimsikiliza kiongozi wa Mbio za Mwenge 2018 (hayupo pichani) siku ya tarehe 07 Oktoba 2018.
Picha na Samwel Mwantona
Alisema uwekezaji katika masuala ya maendeleo unaendana na uhiari katika kupanga kwa kuchagua kipi kianze na baada ya kupanga linafuata suala la utekelezaji wa yale yaliyokubaliwa katika kupanga.
Alisema wanaoshindwa kutekekeleza baada ya makubaliano wanatakiwa kufuatiliwa na kuchukuliwa hatua zinazostahiki ili kuhakikisha wanatimiza yale waliyokubaliana wakati wa kupanga.
Mhandisi Kabeho alisema wakati wa utekekelezaji wa masuala ya maendeleo jamii hujitolea michango ya hali na mali hivyo jamii/wananchi wana haki ya kupata mrejesho wa kile walichochangia kilichopatikana na matumizi yake ili kujenga misingi ya imani na uwazi kwa jamii kujitolea zaidi uwekezaji katika maendeleo yao.
Akizungumzia elimu bure alisema elimu bure haijaondoa wajibu wa wazazi,walezi na jamii kuchangia elimu kwa mfano kuchangia chakula shuleni na kuwanunulia watoto mahitaji ya kielimu.
“Wanafunzi someni kwa bidii” alisema kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 na kuongeza kuwa tumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh:John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure ili watoto wasome na kufaulu vizuri.
Kuhusu ugonjwa wa Malaria bwana Kabeho alisema jamii inatakiwa kuweka mazingira safi ili kuondoa mazalia ya Mbu wanaosambaza ugonjwa huo na magonjwa mengineyo na kuitaka jamii kuwahi kwenda katika vituo vya matababu mara wanapojisikia homa ili kupata vipimo sahihi kwani si kila homa ni Malaria.
Alisema ugonjwa Malaria umekuwa ukiathiri wakina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kusisitiza umuhimu wa mama mjamzito kuhudhuria kliniki yeye na mume wake ili kujenga heshima ya kuwa baba bora katika malezi kwa kuijali familia yake.
“Mume kwenda kiliniki na mke wake wakati mama akiwa mjamzito mtoto anaanza kuhisi upendo wa baba tangu akiwa tumboni” alisema bwana Kabeho.
Pia aliitaka jamii kupiga vita dawa za kulevya kwa kuwataja wote wanaojihusisha na biashara hiyo ili sheria ichukue mkondo wake lengo la kutokomeza biashara hiyo haramu.
Ukiwa katika Wilaya Kilindi Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 ulipokea taarifa za miradi na kukagua mradi wa ufugaji Nyuki na utunzaji wa mazingira katika kijiji cha Mkindi uliogharimu Tsh milioni zaidi ya Tsh milioni 13,ulifungua vyumba vitatu vya madarasa sekondari ya wasichana Kilindi vilivyogharimu zaidi ya Tsh milioni 61.2 na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mnkonde ambapo ujenzi katika hatua iyofikia umegharimu zaidi ya Tsh milioni 35.7.
Kiongozi wa mbio za Mwenge Mhandisi Charles Fransis Kobeho akizindua Mradi wa Madarasa matatu katika shule ya Sekondari ya wasichana Kilindi uliogharimu zaidi ya Tsh milioni 61.2 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi siku ya tarehe 07 Oktoba 2018. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya kilindi Mhe. Sauda Mtondoo. Picha na Samwel D.Mwantona
Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 ulikagua ujenzi wa awamu ya kwanza wa barabara ya Kimembe-Kilwa-Kwadundwa yenye urefu wa km 3.3 na katika awamu ya pili km 8.7 zinatarajiwa kutengenezwa na hadi kukamilika zaidi ya Tsh milioni 142.7 zinatarajiwa kutumika
Mwenge wa Uhuru pia ulikagua na kupokea taarifa ya uendelevu wa miradi iliyowekewa mawe ya msingi na kufunguliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2017
Ukiwa katika mradi wa maji Muungano/Kigwama ambapo mwenge wa Uhuru mwaka 2018 ulipangiwa kuzindua mradi huo lakini tukio hilo halikufanyika kwa sababu ya kutokamilika kwa uwekaji wa pampu yake ya maji kwani iliyokuwepo iliazimwa kwa muda kwa mkandarasi wa mradi.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018 alijiridhisha katika ukamilifu wa miundo mbinu mingine ya mradi kwa kufanya ukaguzi ,baada ya ukaguzi alisema mradi ni mzuri na unaridhisha lakini hauwezi kufunguliwa kwa sasa hadi hapo itakaponunua pampu yake ya maji.
Alisema mradi huo kwa sababu ya ukosefu wa pampu yake ulitakiwa uwekewe jiwe la msingi na kuitaka wizara husika kuharakisha kuleta fedha wilayani Kilindi ili wananchi wa Muungano/Kigwama waweze kupata huduma ya maji kama lengo la mradi lilivyokusudiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda Mtondoo na kulia kwake ni Katibu Tawala Wilaya ya Kilindi Bi. Warda A.Maulidi muda mfupi walipowasili Wilaya ya Handeni kukabidhi Mwenge wa Uhuru Wilayani humo leo tarehe 08 October 2018. Picha na Samwel Mwantona
Imeandaliwa na:
Modi Mngumi-Kilindi
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.