Watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kubainisha na kubuni vyanzo vya mapato ili kufikia malengo ya Halmashauri ya kukusanya shilingi Bilioni 2.3 katika Mwaka wa fedha wa 2018/2019.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi, Ndg. Gracian M.Makota katika kikao na wafanyakazi wa makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya kilichokuwa na lengo la kutambuana na kusikiliza changamoto zinazokabili Idara na Vitengo.
“Naamini kila Idara na Vitengo mmetengeneza makisio ya mwaka wa fedha 2018/19, na mnahitaji fedha ili kutekeza mipango mlojiwekea hivyo kama hakutakuwa na juhudi katika kukusanya mapato mtakapohitaji fedha kwaajili ya mipango yenu” Alisema Ndg. Makota
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Ndg. Gracian M.Makota akizungumza jambo katika kikao na watumishi siku ya tarehe 12/09/2018 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.Picha Afisa TEHAMA wetu
Aliwataka watumishi wote kutosita kumshirikisha katika mambo mbalimbali yanayoweza kusaidia kuinua mapato ya Halmashauri kwakua kila mtumishi anawajibu wa kuhakikisha mianya ya upotevu wa mapato inadhibitwa lakini pia njia za ukusanyaji zinaongezeka.
Akichangia mawazo katika kikao hicho Ndg.Bakari Mnaguzi aliomba ofisi ya mkurugenzi kusaidia ukarabati wa gari ya misitu ili kuweza kudhibiti mapato ya Misitu na Maliasili. Mkurugenzi alipokea ombi hilo na kuaidi kulishughurikia pia alisema Halmashauri ipo katika utaratibu wa kuanzisha Karakana ya kurekebisha magari mabovu ya Serikali hapahapa Wilayani.
Mbali na hayo Mkurugenzi aliwataka watumishi kutatua kero za wananchi wanaofika katika Ofisi zao lakini pia kutofanya kazi kwa mazoea ili kupunguza malalamiko ya wananchi wanaohitaji huduma katika ofisi zilizopo Makao Makuu ya Halmashauri.
Akifafanua zaidi alihitaji watumishi kushirikiana ili kuyafikia malengo ambayo Halmashauri imejiwekea lakini pia viongozi wa Idara na Vitengo kuhakikisha wanawaunganisha watumishi walio chini yao.
Mwisho
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.