Mkuu wa wilaya Kilindi Mh:Sauda Mtondoo amewataka viongozi wilayani hapa kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na hatimiliki za ardhi.
Mh:Mtondoo alitoa wito huo jana wakati akikabidhi hatimiliki za ardhi kwa wananchi na taasisi za serikali wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya hati hizo iliyofanyika katika ofisi za makao makuu ya Halmashauri ya wilaya Kilindi.
Alisema hivi sasa huduma za upatikanaji wa hati za umiliki wa ardhi zimesogezwa karibu na wananchi uamuzi ambao ulifanywa na serikali kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi baada ya kuanzishwa kwa ofisi za ardhi ngazi za mikoa,hivyo ni wajibu wa viongozi wilayani hapa kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuchangamkia fursa hii muhimu.
“Awali wananchi ilibidi wasafiri mpaka Moshi mkoani Kilimanjaro ili kupata hati ya umiliki wa ardhi lakini sasa hatuna budi kuishukuru serikali kwa kusogeza huduma hii hapa katika mkoa wa Tanga na leo hii tunashuhudia wananchi wakikabidhiwa hati zao hapa wilayani” alisema Mh:Mkuu wa wilaya.
Alisema kwa sababu ya umbali wa kutoka Kilindi hadi Moshi wananchi wengi walikuwa wakishindwa kufuatilia hati zao kwa sababu ya gharama za usafiri na nyinginezo na kuishukuru serikali kwa uamuzi wa kusogeza huduma katika ngazi ya mkoa.
Mh:Mtondoo alisema hati za ardhi zinaweza kutumika katika mambo mbalimbali ikiwemo kupata mikopo katika taasisi za kifedha na hatimaye kuweza kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Akizungumza awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilindi bwana Gracian Makota aliwapongeza wananchi waliopata hati za ardhi na kuwataka wananchi wengine kujitokeza kupata hati hizo ili kuwa wamiliki halali wa ardhi kisheria.
Akitoa takwimu afisa ardhi wilaya Kilindi bwana Natus Manumbu alisema jumla ya hati 49 zimeidhinishwa na kusajiliwa na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Tanga ambapo kati ya hizo 21 ni Hati za viwanja vya serikali na 28 ni Hati za viwanja vya wananchi.
Hafla hii fupi ilihudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali kutoka wilayani na mkoani akiwemo Kamishna wa ardhi msaidizi mkoa wa Tanga bwana Tumaini Gwakisa ambae aliambatana na Viongozi waandamizi kutoka Ofisini kwake.
Modi Mngumi-Kilindi
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.