Waheshimiwa madiwani katika Halmashauri ya wilaya Kilindi wametakiwa kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro iliyopo katika maeneo yao badala ya kuwa chanzo cha migogoro hiyo.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa wilaya Kilindi Mh:Sauda Mtondoo wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha ufunguzi wa baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Alisema Wilaya Kilindi inakabiliwa na migogoro ikiwemo ya mipaka,wakulima na wafugaji na ipo iliyokwisha,iliyopo katika hatua nzuri ya utatuzi na mingine inaendelea kushughulikiwa katika ngazi za juu,hivyo waheshimiwa madiwani watumie hekima,busara na vipaji wwalivyojaaliwa na mungu kuhakikisha migogoro inamalizika kwa Amani.
Alisema kazi iliyopo kwa sasa ni kuleta maendeleo kwa wananchi na changamoto zilizopo wilayani zitumike kama fursa za kusogeza mbele wilaya kimaendeleo na sio sehemu ya kulalamika na kuona kwamba haiwezekani kuvuka katika jambo hilo.
Mh:Mkuu wa wilaya Mtondoo alisema wananchi wana matumaini makubwa ndiyo maana waliwaamini na kuwachagua,hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuchapa kazi kwa maendeleo ya jamii.
“Tuchape kazi na kila mmoja aone ana wajibu wa kuhakikisha anakwenda kuwatumikia wananchi,sote tusimame kama timu moja kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya Kilindi”alisema Mh:Mkuu wa wilaya.
Akizungumzia kuhusu uhaba wa vyumba vya madarasa kwa kidato cha kwanza alisema waheshimiwa madiwani ambao ndiyo wenyeviti wa kamati za maendeleo katika kata wahakikishe wanashirikiana na viongozi wote katika kata zao ili kuhamasisha maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa ili vijana waliochaguliwa kidato cha kwanza waweze kujiunga na masomo kama ilivyokusudiwa.
Alisema kila kata iwe na mpango mkakati wa kudumu kwa kuweka mipango mapema mara tu vijana wanapojiunga darasa la kwanza kwa uongozi wa kata kuanza kufikiria mahitaji ya kielimu mapema na isiwe kama zimamoto.
Waheshimiwa madiwani katika kikao hicho pia waliapishwa kiapo cha uadilifu kwa mujibu wa maadili ya viongozi wa umma na kumchagua Mh:idrisa Mgaza kuwa mwenyekiti wa Halmashauri na makamu wake Mh:Ndeiya Seiya
Modi Mngumi-Kilindi
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.