Programu ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu (FORVAC) imesaidia kuviwezesha vikundi 5 vya ufugaji Nyuki wilayani Kilindi mizinga 100 na vifaa kinga mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Tsh milioni 26.1.
Akikabidhi vifaa hivyo jana mjini hapa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi bwana Gracian Makota,Mratibu wa Progam ya FORVAC kongani ya Tanga bwana Petro Masolwa alivitaja vikundi hivyo ni kutoka katika vijiji vya Mafisa , Madukani Majengo,Kwamwande,Tuliani Kwedijelo na Komnazi.
Alisema lengo la FORVAC ni kusaidia kuongeza thamani ya mazoa ya misitu ikiwemo Asali na mazao yake ili kuongeza kipato cha wafugaji Nyuki na hatimaye kuondoa au kupunguza umaskini kwa kuboresha kipato cha kaya na Taifa kwa jumla.
Akipokea vifaa hivyo Mkurugenzi Mtendaji Bwana Makota ameishukuru progam FORVAC kwa kuwezesha wananchi wa katika Halmashauri yake na vifaa vilivyotolewa vitasaidia wafugaji Nyuki kufuga kisasa na kuongeza mazoa ya asali.
Alisema ufugaji Nyuki unaendana na suala zima la utunzaji wa mazingira na kutoa wito kwa taasisi na vijiji katika Halmashauri ya Wilaya Kilindi kuongeza kasi ya utunzaji mazingira kwa kupanda miti na kuacha kukata miti hovyo.
Program ya FORVAC iliyoanza mwaka 2018 na kukamilika mwezi wa 5 mwaka 2022 imewezesha wafugaji Nyuki wilayani Kilindi kuongeza thamani ya mazao ya Nyuki na kuwezesha kuongeza thamani ya mazao ya Asali ambapo kwa mujibu wa Afisa Nyuki wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi bwana Shilibe Metipoi kwa mwaka 2021/22 jumla ya Tani 2.7 zilipatikana na wafugaji waliweza kupata kiasi cha Tsh mil 27.
Alisema FORVAC imefanikisha urudishaji wa miche ya miti katika maeneo yasiyo na miti katika msitu wa hifadhi wa kijiji cha Mnkonde wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa usimamizi misistu ambapo miche 11,600 ilipandwa katika sehemu yenye uerfu wa kilomita 13 na maeneo ambayo yaliharibiwa yenye ukubwa wa Hekta 3.75.
MODI MNGUMI KILINDI
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.