Benki ya NMB imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni kumi kwaajili ya mikopo kwa Wakulima wa mazao mbalimbali ndani ya Wilaya ya Kilindi katika mwaka wa fedha 2020/2021, ameyasema hayo Meneja Mahusiano Biashara na Kilimo Benki ya NMB Ndg. Samson Siyengo leo tarehe 02.08.2020.
Ndg. Siyengo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wakulima wa kata ya Mvungwe na Kibirashi katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwakutanisha wawezeshaji wa Kilimo (NMB, PYXUS na PASS) na wakulima.
Katika kuhakikisha kuwa wakulima wanafanikiwa na wanapata manufaa katika kilimo kampuni ya PYXUS itasimamia utoaji wa mbegu Kwenye vyama vya ushirika pamoja na ununuzi wa zao la Alizeti, Benki ya NMB itashughurikia kutoa mikopo ya mitaji na pembejeo za Kilimo, Kampuni ya PASS itamsaidia mkulima kupata mikopo ya kifedha na pembejeo za kilimo.
“Sasa Kilindi tupo katika hatua ya kuzalisha alizeti zitakazo uzwa nje ya nchi” aliyasema hayo Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kilindi Ndg. Gracian Max Makota alipokuwa akifungua mafunzo haya kituo cha Songe kilicho fanyia mafunzo Ukumbi wa Halmashauri tarehe 01.08.2020.
Aidha Ndg. Samwel Andrew Klure ambaye ni Meneja kampuni ya PYXUS Wilaya ya Kiteto na Kilindi, ambayo inajuhusisha na ununuzi wa mazao ya Alizeti ndani ya Wilaya ya Kilindi. Amesema kampuni imeandaa vifaa na mashine za kubangua alizeti pamoja mifuko ya kubebea mazao kutoka shamba hadi eneo la soko.
Aidha Afisa maendeleo ya biashara Kampuni ya PASS Ndg. Emilian Barongo ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Kilindi chini ya Mkurugenzi Mtendaji Ndg.Gracian M.Makota kwa kuwaunganisha wadau mbalimbali kwaajili ya kuinua maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo wakulima walioshiriki mafunzo haya wameipokea kampuni ya PYXUS kwa mikono miwili kutokana na bei wanayoitumia kununua zao la alizeti lakini pia msaada wa mashine za kubangua alizeti zilizotolewa katika vyama vya Ushirika.
Habari hii imeandaliwa na :
Samwel Daniel Mwantona
Afisa TEHAMA
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.