Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe.Sauda Salum Mtondoo ahitimisha zoezi la utoaji Mikopo kwa vikundi vya uzalishaji mali vya vijana kwa kukabidhi pikipiki kumi(10) kwa vikundi vitatu katika halfa fupi iliyofanyika katika viwanja vya Makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Kilindi Songe,siku ya alhamisi saa 3:00 asubuhi tarehe 31.01.2019
Akikikabidhi pikipiki hizo zenye thamani ya fedha kiasi cha shilingi za kitanzania milioni ishirini ambazo zimetokana na asilimia nne (04) ya mapato ya ndani ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mkuu wa wilaya huyo akikabidhi pikipiki hizo alisizitiza mambo mbalimbali kama kuzingatia sheria za usalama barabarani, kufanya kazi kwa malengo ili kusaidia mkopo uwe wenye tija na endelevu kwa vikundi vingine pasipo kuwa na riba yoyote ya mkopo huo.
Aidha Mhe.Mkuu wa wilaya aliendelea kuwasisitiza vijana waliopewa huo kuwa waaminifu, katika kufanya marejesho ya Mkopo ili kuweza kutoa fursa kwa vijana wengine kuweza kupata mikopo kutokana na fedha za marejesho hayo.
Mhe.Mkuu wa wilaya alisema kuwa uhamasishaji ufanyike zaidi kwa vijana ambao hawakupata fursa hiyo ili waweze kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali kwa kusajiliwa halmashauri na kuweza kutuma maombi ya mkopo ili kuondokana na shughuli zisizo endana na maadili ya kijamii kama wizi, ukabaji, uzururaji, utumiaji wa madawa ya kulevya na vitendo vingine vinavyoendana na hivyo na badala yake wajikite kwenye kufanya shughuli zenye kuleta maendeleo katika wilaya na Taifa kwa ujumla.
Pia aliwaasa vijana waendesha boda boda Kilindi kutowarubuni wanafunzi wakike kwa kuwapatia lifti na kuwapa ujauzito, badala yake wawapende, wawajali, wawathamini na kuwa msaada kwao ili kuwasaidia kutimiza malengo yao ya kupata elimu.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Mussa Semdoe kwa upande wake alisisitiza usimamizi wa mapato ya ndani ili kuweza kutenga kirahisi asilimia kumi (10%) ya makusanyo ya ndani ili kuendelea kutoa mikopo kwa vikundi wanawake, vijana na walemavu kwa mujibu wa kanuni na sheria, pia aliahidi kuwa halmashauri itasimamia na kuhakikisha kuwa asilimia kumi ya mapato inatengwa na kuwa fikia wananchi wa Kilindi kwa kupitia vikundi vya uzalishaji mali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi Ndg Gracian M.Makota aliwahamasiha vijana wilaya nzima kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo ili viwezekombolewa na mikopo inayotokana na asilimia kumi (10%) ya fedha za makusanyo ya ndani kwaajili ya vikundi vya kinamama, vijana na walemavu.
Lakini pia Mkurugenzi mtendaji alisisitiza kuwa walemavu nao wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kwakujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali ili kuweza kunufaika na mikopo itokanayo na asilimia mbili (02%) ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri.
Afisa Maendeleo ya vijana ndg Godfrey Msuya alitoa ufafanuzi wa jinsi mikopo ya Halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii ilivyotolewa na kueleza kuwa kwa kipindi hicho cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ilifanikiwa kutoa mikopo ya yenye thamani ya jumla ya fedha za kitanzania shilingi milioni 80 kwa vikundi vya wanawake na vijana
Ndg Msuya alisema kuwa hafla hiyo ya ugawaji wa pikipiki ni hitimisho la mikopo iliyokwisha tolewa katika vikundi mbali mbali vya uzalishaji mali.
Kwa niaba ya vijana walionufaika na mkopo Ndg.Ally Kifyambo aliishukuru serikali ya kwa kuwawezesha mkopo usio na riba na aliahidi kuwa, watakuwa waaminifu katika kufanya marejesho ya mkopo huo na kuwahimiza vijana wenzao kuweza kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ili waweze kutekeleza shughuli zao mbalimbali za maendeleo na kuinua kipato chao.
Hafla hiyo ya kukabidhi pikipiki kwa vikundi vya vijana iliambatana na shughuli ya kumkabidhi Mwekahazina wa Wilaya Gari jipya la Halmashauri aina ya Nissan Double Cabin yenye namba za usajili SM 12622 lililonunuliwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri kwaajili ya shughuli za ukusanyaji mapato,zoezi hili la kukabidhi gari hilo lilifanywa na mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mussa Semdoe katika viwanja vya makao makuu ya Halmashauri Songe
Na: Ulirch P.Laswai
Afisa TEHAMA
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.