Mkuu wa wilaya ya kilindi Mhe.Sauda Salumu Mtondoo akabidhi hundi za kuwezesha vikundi vya wanawake kiasi cha shilingi milioni thelathini na mbili (32,000,000/=) katika kuwakwamua wanawake kiuchumi kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe 08 machi 2018, ambapo katika maadhimsho hayo yeye alikuwa ndiye mgeni rasmi.
Alipokuwa akiwakabidhi hundi hizo aliagiza vikundi hivyo vihakikishe kuwa vinatumia fedha hizo kwa shughuli za kiuchumi(uwekezaji) ili kuinua kipato chao na jamii ya Kilindi kwa ujumla na si vinginevyo.
Mkuu wa wilaya Mhe.Sauda Salumu Mtondoo akimkabidhi mmoja wa wakilishi wa kikundi cha wanawake, kushoto kwake ni Mkurugenzi mtendaji Ndg Clemence A.Mwakasendo na kulia kwake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mhe.Sempule
Hata hivyo halmashauri imekuwa ikitoa fedha kila mwaka kuwezesha vikundi vya kinamama na vijana kwa kutekeleza agizo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakisha kuwa kila halmashauri inatoa asilimia nne (04%) ya mapato yake ya ndani kuwezesha vikundi hivyo.
Naye Meneja wa benki ya NMB Tawi la Kilindi ndugu Phillemon Tarimo aliwapongeza wanakawake kwa maadhimisho ya siku hiyo pamoja na kuwashauri wanawake kujiunga na kusajili vikundi mbalimbali vya kiuchumi ili kurahisisha uwezeshwaji wa kifedha kwenye benki hiyo.
Meneja wa Benki ya NMB tawi la Kilindi Ndg Philemon Taimo (aliyesimama) akitoa elimu kwa vikundi vya kinamama
Picha na Clement A.Moshi
Aidha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani hufanyika kitaifa kila tarehe 08 mwezi Machi ya kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu yalifanyikia wilayani Mikindani katika huko Mkoani Mtwara.
Maadhimisho hayo yaliambatana na kauli mbiu isemayo “kuelekea uchumi wa viwanda, tuimarishe usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake vijijini”
Mwisho wa maadhimisho hayo Mkuu wa wilaya Mhe.Sauda Salumu Mtondoo aliongoza katika zoezi la kuchangia damu ili kuokoa maisha ya kinamama na jamii yote ya Kilindi kwa ujumla, ambapo watumishi na baadhi ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho hayo walishiriki kujitolea damu ambayo ilipelekwa katika Hospitali Teule ya Wilaya (CDH)
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.