Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela jana ametoa ahadi ya Shilingi laki mbili kwa kila mwanafunzi wa kidato cha nne atakayepata ufaulu wa daraja la kwanza katika Shule ya Sekondari ya wasichana Kilindi.
Mhe. Shigela alitoa ahadi hiyo alipofanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa madarasa katika shule hiyo, ikiwa ni kuwapa hamasa wanafunzi hao wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne mapema mwezi Novemba. Hii ni kutokana na shule hiyo kukosa ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani wa Taifa kidato cha nne mwaka jana.
“Tunajipanga kuangalia ni namna gani kila mwanafunzi anaweza kuhitimu lakini si kuhitimu tu bali kuhitimu kwa ufaulu mkubwa” alisema Mhe. Shigela na kuongezea kwamba “ Kila mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza katika mtihani wa Taifa nitampatia laki mbili bila kujali wangapi mtapata daraja hilo”.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akizungumza na wanafunzi wa kidatoa cha nne Shule ya Sekondari ya wasichana Wilayani Kilindi (hawapo pichani) siku ya tarehe 27/09/2018, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda Mtondoo. Picha na Samwel Mwantona
Maneno hayo ya Mkuu wa Mkoa yalipokelewa kwa shangwe na wanafunzi hao kama ishara ya kuongeza juhudi katika masomo yao ilikupata zawadi hiyo iliyoaidiwa na kiongozi huyo wa Mkoa wa Tanga.
Hata hivyo Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bi. Zena Said aliwahamasisha wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwani wataalam na viongozi wa aina mbalimbali wa kizazi kijacho watatokana na wao, hivyo aliwaasa kuepukana na vishawishi lakini pia mambo yanayoweza kuathiri elimu yao.
Mbali na Mradi wa madarasa katika shule hiyo Mhe.Shigela alikagua Mradai wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mnkonde lakini pia Mradi wa ujenzi wa maji Kata ya Msanja (Mradi wa Kwinji Muungano).
Aidha akiwa katika mradi wa Zahanati Mkuu wa Mkoa aliupongeza uongozi wa wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya Mhe.Sauda Mtondoo kwa kushirikiana vyema na wananchi hadi kufikia hatua ya kupaua jengo hilo la Zahanati. Lakini pia alihitaji diwani wa Kata hiyo Mhe. Mkomwa kueleza changamoto, ambapo diwani huyo aliitaji msaada katika kulikamilisha jengo hilo la Zahanati.
Naye Mkuu wa Mkoa kupitia maombi ya diwani huyo aliiahidi kutoa mifuko sabini ya saruji lakini pia rangi ya kwaaji ya jengo hilo, lakini pia Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kilindi walichangia mifuko 30 kila mmoja ili kuunga mkono juhudi za wananchi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mnkonde alipokuwa akikagua Mradi wa Zahanati ya Kijiji hicho siku ya tarehe 27/09/2018. Kulia ni Katibu Tawala Mkoa Bi. Zena Saidi na kushoto ni Mkuu wa Wilaya Mhe. Sauda Mtondoo. Picha na Samwel Mwantona
Mbali na kukagua Mirada hiyo ya maendeleo Mhe. Shigela alizindua chuo cha Ufundi Stadi ( VETA ) kilichojengwa kata ya Mabalang’a. Ambapo ujenzi wa chuo hicho cha ufundi chini ya Ufadhili wa shirika la “World Vission” ulianza mwaka 2002 na umegharimu zaidi ya kiasi cha Shilingi milioni 350 mpaka kukamilika kwake.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigela akiwasili katika eneo la chuo cha Ufundi Stadi ( VETA ) kilichopo kata ya Mabalang’a wilaya ya Kilindi siku ya tarehe 27/09/2018. Kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Tanga Bi. Zena Said na Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda Mtondoo. Picha Samwel Mwantona
Akiwa katika uzinduzi huo alitoa aliomba jamii inayokizunguka chuo hicho na wanakilindi wote kuitumia fursa ya uwapo wa chuo hicho vizuri kwa kuhakikisha wanapata elimu itakayowasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Pia alikagua vikundi mbalimbali vya wajasiriamali waliojitokeza pamoja na banda la wanafunzi wa shule ya msingi waliondaa kazi mbalimbali za sanaa katika eneo hilo. Hata hivyo Mkuu wa mkoa alivutiwa sana na uzalishaji wa zao la mhogo unaofanyika katika eneo la kilindi, hii ni kutokana na aina ya mhogo uliokuwa unazaidi ya kilo 10 alionyeshwa katika banda hilo la wakulima.
Mwisho Mkuu wa Mkoa alifanya mkutano na kusikiliza kero za wananchi Kata ya Kwediboma. Katika mkutano huo wananchi nane walipata fursa ya kuuliza maswali zaidi ya ishirini ambapo yalipata majibu ya moja kwa moja kutoka kwa Mkuu wa Mkoa pamoja na wataalam wa Halmashauri.
Katibu Tawala Wilaya ya Kilindi Bi. Warda A.Maulid akitambulisha viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa Chuo cha Ufundi VETA kata ya Mabalang’a Wilaya Kilindi siku ya tarehe 27/09/2018. Picha na Samwel Mwantona
Miongoni mwa kero iliyowasilishwa na wananchi hao ilikuwa ni pamoja na upungufu wa madarasa katika shule ya msingi Uwanja wa Ndege hii ni kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo shuleni hapo. Hari ambayo ilimgusa sana Mkuu wa Mkoa na kutoa ahadi ya mabati 130 pamoja kufanya changizo kwa viongozi wa Halmashauri na kupata pesa na vifaa vyenye jumla ya thamani zaidi ya shilingi laki nne.
Aidha Mkuu wa Mkoa aliupongeza uongozi wa Wilaya na Halmashauri chini ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Sauda Mtondoo kwa namna unavyotekeleza na kusimamia kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya.
Na Mwandishi
Samwel D.Mwantona ( A/TEHAMA)
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.