Mahakama ya Wilaya Kilindi imemhukumu Elton Chrisopher (19) mkazi wa kijiji cha Kigwama kata ya Msanja kwenda jela miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka 6.
Hukumu hiyo ya kesi ya Jinai Na.97 ya mwaka 2020 imetolewa Aprili 13 mwaka huu na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Mariamu Mfanga
Akitoa hukumu hiyo Hakimu mkazi Mfawidhi amesema mahakama imemhukumu mshtakiwa kifungo hicho baada ya upande wa mashtaka kuweza kuthibitisha shtaka pasipo kuacha shaka yeyote.
Amesema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka hilo kufuatia uthibitisho wa ushahidi uliotolewa na daktari baada ya kumfanyia uchunguzi binti aliyebakwa pamoja na mashahidi waliofika kutoa ushahidi wakiwemo wazazi,walimu na majirani,ushahidi ambao haukuacha shaka yeyote.
Awali imedaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa polisi Koplo Sefu Makono kuwa mshtakiwa alimbaka binti huyo wa miaka 6 Oktoba 31 mwaka jana katika kijiji cha Kigwama kilichopo kata ya Msanja wilayani Kilindi.
Mwendesha mashtaka huyo ameendelea kudai kuwa mshtakiwa ambaye alikuwa ni mtumishi wa nyumbani kwa binti aliyembaka alimfanyia kitendo hicho baada ya kumpeleka katika nyumba mbovu iliyopo karibu na nyumbani kwa mtoto huyo.
Koplo Sefu amedai kuwa binti huyo aligundulika amebakwa kufuatia jirani wa nyumba anayoishi mtoto huyo ambaye ni mwanamke kumuona binti huyo akiwa amelala na hakuwa akicheza na wenzake kama kawaida yake na alipomchunguza aligundua mtoto huyo akiwa na damu katika sehemu zake za siri.
Imeendelea kudaiwa kuwa baada ya tukio hilo taarifa ilitolewa polisi na mtoto alipelekwa hospitali ya wilaya Handeni ambapo vipimo vya daktari vilithibitisha kuwa binti alikuwa amebakwa.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi Mariam Mfanga ametoa wito kwa wakazi wa Wilaya Kilindi kutoa ushirikiano pindi zinapojitokeza kesi kama hizo ili kukomesha vitendo vya ukatili katika jamii.
MWISHO
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.