Wazazi na walezi wilayani Kilindi watakiwa kuwekeza katika elimu ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila ubaguzi wa jinsia, rangi na ulemavu kwani Elimu ndio msingi wa maisha na urithi ulio bora kwa watoto.
Hayo yalisemwa na Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda S.Mtondoo katika Hotuba yake iliyowasilishwa na Katibu Tawala Wilaya ya kilindi Dkt. Phillis M.Nyimbi katika maadhimisho ya siku ya mototo wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika Shule ya Msingi Kimembe siku ya tarehe 21/06/2018.
Mtondoo alisema watoto wanapohitimu elimu ya msingi au sekondari na kukosa ufaulu wa juu na kuendelea na masomo ya juu isiwe ni mwisho wao kielimu, bali wazazi na walezi wawatafutie vyuo vya ufundi mbalimbali jambo litakalo wasaidia kujitegemea na kujiajiri hata kutoa ajira kwa jamii hata kufikia uchumi wa viwanda.
“ Ili kufikia uchumi wa viwanda, wazazi na walezi hakikisheni mnawekeza elimu kwa watoto hasa wakiwa wadogo maana elimu ndio msingi wa maisha na urithi ulio bora kwa watoto kwani huongeza ujuzi na maarifa” Alisema Mhe. Mtondoo katika hotuba yake iliyosomwa na Dkt. Nyimbi.
Aidha wazazi wametakiwa kutokomeza ndoa na mimba za utotoni, kuwekeza katika lishe bora, huduma bora za Afya, maji, kuwatetea watoto katika suala la uhai, unyanyasaji, ulinzi nma maendeleo yao kwa ujumla na kuimarisha mila na desturi zinazokubalika ma kukabiliana na utandawazi.
Hata hivyo Shirika Binafsi la World Vision lililoandaa sherehe hizo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Wilaya ya Kilindi, lilitoa zawadi ya mabegi zaidi mia moja kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao, Walimu na Mratibu kata, kata ya Kilwa tarafa ya Mgera, Wilaya ya Kilindi.
Katibu Tawala Wilaya ya KIlindi Dkt. Phillis Nyimbi akimkabidhi zawadi ya begi mwanafunzi Fatuma Hamza Hamisi wa Shule ya Msingi Kimembe. Siku ya maadhimisho ya Mtoto Afrika Kiwilaya yaliyofanyika Shule ya Msingi Kimembe, tarehe 21 juni 2018.
Mbali na World Vision shirika la Amref walitoa zawadi ya viti viwili vya magurudumu kwa walemavu ( wheel chair ). Walemavu hao waliopata zawadi hizo ni Saumu Ramadhani mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Uwanja wa Ndege pamoja na Mazua Saidi Mtula wa darasa la nne katika shule ya Msingi Kilwa.
Zawadi hizo zilikabidhiwa kwa watoto hao na Dkt. Phillis Nyimbi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda S.Mtondoo. Mbali na hivyo alitoa shukrani kwa wadau hao kwa kuona umuhimu wa kuwekeza katika Elimu kwani ni Msingi wa Maendeleo katika nchi.
Katibu Tawala Wilaya Mhe. Dkt. Phillis Nyimbi akiwakabidhi zawadi ya viti vya magurudumu wanafunzi walemavu, Saumu Ramadhani (wa kwanza kushoto) darasa la sita Shule ya Msingi Uwanja wa Ndege pamoja na Mazua Saidi Mtula (wa pili) , darasa la nne shule ya Msingi Kilwa.
Kaimu Mkurugenzi Bi. Dafroza Mkenda aliiasa jamii kuhakikisha wanaswapa watoto haki ya elimu maana ni wajibu wa mzazi kwa mototo na wala sio ombi, hivyo jamii imetakiwa kushirikiana na juhudi za Serikali kwa kuhakikisha inaandaa miundo mbinu mizuri ya Shule.
Mwanafunzi Lidia Yoramu wa Darasa la saba Shule ya Msingi Kimembe alitoa Shukrani kwa Serikali kwa kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi hadi Sekondari, mbali na hivyo alitoa shukrani kwa shirika la World Vision kwa misaada yake. Maneno hayo aliyasema alipokuwa akisoma Risala Mgeni Rasmi.
Maadhimisho ya siku ya mototo wa Afrika huaadhimishwa barani Afrika tarehe 16 juni kila mwaka. Siku imeteuliwa rasmi kwaajili ya kumbukumbu ya mauaji ya watoto wa shule huko SOWETO Afrika kusini hivyo nchi wanachama wa umoja wa nchi huru za Afrika wakaweka adhimio la kuhadhimishwa siku hiyo.Japo kiwilaya yalifanyika tarehe 21 juni.
Wanafunzi wa shule ya Msingi Kimembe wakionyesha Kipaji cha kucheza Ngoma za asili Mbele ya Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto Afrika siku ya tarehe 21 juni 2018.
Mwisho.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.