Wilaya ya Kilindi imefanikiwa kuzindua Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Kilindi (MMEK) utakaosaidia kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu bora wilayani hapa.
Uzinduzi wa mfuko huo umefanyika jana katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Kilindi ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya Mh:Abel Yeji Busalama
Akizindua mfuko Mh:Busalama amesema mfuko huo utakuwa mkombozi wa maendeleo ya elimu kwa jamii nzima ya Kilindi na utawawezesha kukabiliana na changamoto za kielimu katika shule za msingi na sekondari wilayani hapa
Awali akisoma taarifa ya uanzishwaji wa Mfuko wa Maendelo ya Elimu Kilindi (MMEK) Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bwana Gracian Makota amesema pamoja na jitahada za serikali za kuboresha elimu kupitia programu mbalimbali bado changamoto zimeendelea kuwepo ikiwa ni pamoja na uwezo wa kifedha wa serikali ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Bwana Makota katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Elimu Msingi Wilayani hapa Bwana Danstan Ntauka amesema nia ya kuanzisha mfuko katika Halmashauri imekuja kwa lengo la kuongeza nguvu na uwezo katika kukabiliana na changamoto za kielimu kwa kushirikisha wananchi na wadau mbalimbali.
Akitaja malengo ya Mfuko amesema ni kuhamasisha na kuboresha maendeleo ya elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Ufundi Stadi katika Halmashauri, Kuboresha miundo mbinu ya elimu, kufanya ufuatiliaji wa shughuli za kielimu, kudhamini wanafunzi wahitaji,kusaidia serikali kurekebisha ikama na kufanikisha malengo ya mfuko.
Akizungumzia uongozi Bwana Makota amesema Mfuko utakuwa na Bodi ya Wadhamini wasiopungua 4 na wasiozidi 8 watakaoteuliwa na Halmashauri ambapo Mwenyekiti wa Bodi atateuliwa na mlezi wa Mfuko ambaye ni Mh:Mkuu wa Wilaya.
Akivitaja baadhi ya vyanzo vya mapato vya mfuko amesema kuwa ni misaada kutoka wahisani, michango kutoka Halmashauri na wananchi, ruzuku mbalimbali na mikopo.
MODI MNGUMI
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.