Jitihada za serikali za kuwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za kifedha zimeanza kuzaa matunda kwa wakazi wa kata ya Kilwa Wilayani Kilindi ,ambao kwa hiari wameamua kujiunga katika vikundi hivyo na kufanikiwa kuweka,kukopeshana na kugawana hisa na michango yao waliojiwekea katika kipindi cha mwaka mmoja.
Hayo yalibainishwa na wanachama wa vikundi vya Kwesongo,Kimembe Centre na Kangama mwishoni mwa wiki katika shule ya msingi Kimembe wakati wa sherehe za mwaka mmoja wa mafanikio ya vikundi hivyo tangu vilipoanzishwa.
Wanavikundi hao katika risala zao walisema tangu kuanzishwa kwa vikundi hivyo mwaka jana wameweza kupata mafanikio mengi ikiwemo kuweza kusomesha watoto,kuongeza kipato cha kaya,kuanzisha na kuendeleza miradi midogo midogo na hata kusaidia watoto walio katika mazingira magumu na walemavu.
Waliendelea kusema wanaishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mh:Rais mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweka sera ya kuwezesha jamii kuwa na huduma ndogo za kifedha ambayo imekuwa na manufaa kwa watu wenye vipato vidogo haswa wanawake ambao wamekuwa wakikabiliwa na majukumu mengi ya ulezi wa watoto na kuongeza kipato cha familia.
Akizungumza katika sherehe hizo Mh:Diwani wa kata ya Kilwa Bakari Honelo aliwataka wakina baba kuwahamisha wake zao kujiunga na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha kwani ni mkombozi wa kaya katika kupambana na umaskini.
Alisema wanawake wakiwezeshwa wanaweza na ndiyo maana hata Halmashauri kupitia michango ya asilimia kumi ina asilimia maalum kwa ajili ya kuwezesha wanawake kupata mikopo.
Akiongea katika sherehe hizo Bwana Godfrey Msuya kwa niaba ya Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Kilindi alisema vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ni mkombozi na hakuna haja ya wananchi kusita kujiunga kwani serikali imekuwa ikijitahidi kuwasaidia wananchi wake kwa kuanzisha sera mbalimbali za kuwakwamua kiuchumi.
Alisema vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za kifedha zinaweza kutatua changamoto za kimaisha kwa kuongeza kipato katika familia na kuwatak wanavikundi kujenga utamaduni wa kuwekeza katika huduma za afya kabla ya kuugua kwa kukata bima za afya kwani afya ndio mtaji wa kila kitu.
Alisema bila afya nzuri hata mwanachama hataweza kuzalisha kwa kuwa ni mgonjwa hivyo ni vizuri kukata bima za afya mapema wakati afya ni nzuri ili kaya iwe na uhakika wa matibabu mwaka mzima hata kama wakati mwanakaya anaugua hakuna fedha bima itaweza kumsaidia.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.