Wakazi wilayani Kilindi wametakiwa kuendeleza mila na desturi zisizokuwa na madhara kwa jamii ambazo zinalenga kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Ushauri huo ulitolewa na Bi.Aneta Helderson katika kijiji cha Lusane wakati wa utoaji mafunzo ya kuachana na mila ya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike inayofanywa na baadhi ya makabila wilayani hapa.
Alisema jamii inazo mila nzuri ambazo hazina madhara kwa wanawake na watoto wa kike mila hizi zinapaswa kuendelezwa lakini mila ya ukeketaji ambayo imekuwa na madhara makubwa kiafya kwa walengwa wake inapaswa kuachwa ili kulinda utu na heshima ya makundi ya watu wanaofanyiwa mila hiyo.
Alisema elimu zaidi inapaswa kutolewa kwa jamii na itachukua muda watu kuachana na vitendo hivi kwani vimekuwa vikifanyika kwa muda mrefu na kurithishwa kizazi hadi kizazi.
Akitoa mada ya ukeketaji na madhara yake katika mafunzo hayo Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya Kilindi bwana Oscar Kiondo alisema jamii inapaswa kuacha mila ya ukeketaji kwani haina faida na badala yake imekuwa ikwasababishia maumivu na masongo wa mawazo walengwa wake.
Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaendelea kuelimisha jamii kuachana na mila hii potofu katika jamii na kuzitaka jamii zinazofanya mila hii kubadilika kwani yapo mambo mengi yamebadilika hivyo hata mila ya ukeketaji inaweza kubadilika kwa watu kuiacha kabisa.
Akizungumza katika mafunzo hayo Bibi Janeth Kamunyu alisema ukeketaji umethibitishwa na madaktari kuwa una madhara makubwa kiafya kwa watu wanaofanyiwa mila hii,hivyo jamii haina haja ya kuendeleza mila hii kwani zipo mila nyingi nzuri za kuendelezwa na jamii ikawa na urithi mzuri wa mila amabazo ni nzuri na kufaa kuendelezwa.
Naye mzungumzaji mwingine katika mafunzo hayo Bibi Naomi Mogen alisema hata kama watu wanaofanyiwa vitendo vya ukeketaji hawaoni madhara yake lakini wanapaswa kuachana na mila hiyo kandamizi kwa wanawake na watoto.
Wakitoa maoni katika mafunzo hayo baadhi ya washiriki walisema wanaume ndio kiini cha mabadiliko katika kuacha mila ya ukeketaji kwa wanawake na watoto wa kike.
NA MODI MNGUMI-KILINDI
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.