Halmashauri ya wilaya Kilindi imefanikiwa kutoa mkopo wa Pikipiki 10 kwa vikundi 2 vya vijana wenye thamani ya Tsh milioni 23.5.
Akikabidhi Pikipiki hizo kwa vikundi hivyo Mh:Mbunge wa Jimbo la Kilindi Bw.Omari Kigua alisema serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mh:Rais Dk John Pombe Magufuli imedhamiria kuwasaidia wananchi wake wakiwemo vijana kwa kutoa mikopo isiyo na riba.
Alisema mikopo inayotolewa na Halmashauri ni kwa ajili ya vijana wote na kuongeza kuwa wanaokopeshwa wakifanya vizuri katika marejesho watatoa fursa kwa vijana wengine kupata mikopo
“Wanakilindi wote wanahaki sawa ya kupata asilimia kumi inayotokana na mapato ya wilaya Kilindi”Alisema Mh:Kigua.
Mh:Kigua pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilindi Bw.Gracian Makota na timu yake ya wataalam kwa jitihada wanazozifanya katika kushughulikia changamoto mbalimbali za kimaendeleo zinazowakabili wanakilindi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Bw.Gracian Makota akizungumza katika makabidhiano ya Pikipiki aliwataka vijana kujikita katika sekta nyingine za uzalishaji mali kama vile useremala na kuanzisha viwanda vidogo vidogo badala ya kutegemea boda boda pekee.
Alisema fursa za kiuchumi zipo nyingi na vijana kama kundi muhimu katika kujenga uchumi wanapaswa kuzitumia fursa hizo ili waweze kujiajiri na hatimaye kufikia lengo la serikali la kuhakikisha tatizo la ajira kwa vijana linapungua.
Naye Mratibu wa dawati la Uwezeshaji wananchi kiuchumi Halmashauri ya wilaya Kilindi bw.Godfrey Msuya alivitaja vikundi vilivyopatiwa Pikipiki hizo ni kutoka katika kijiji cha Kwastemba ambavyo ni Farasi na Wachakarikaji ambavyo vyote kwa pamoja vina jumla ya wanachama 20 na kuongeza kuwa kikundi cha Farasi kimepata Pikipiki 8 na Wacharikaji 2.
Alisema miongoni mwa vigezo vya kupata mkopo wa Pikipiki ni kila mwanakikindi awe amepata mafunzo ya kuendesha Pikpiki na kuwa na leseni ya udereva wa chombo hicho.
Bwana Msuya alisema katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi sasa Halmashauri imefanikiwa kutoa mkopo wenye thamani ya Tsh milioni 66 kwa vikundi 14,kati ya hivyo 10 ni vya wanawake,1 cha walemavu na 3 ni vya vijana.
Habari na: MODI MNGUMI-BOKWA
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.