Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Mhe. Sauda S.Mtondoo leo tarehe 08.05.2019 amezuia uuzaji wa mazao ya chakula nje ya Wilaya kwa lengo la kuhakikisha kuwa Wilaya inakuwa na chakula cha kutosha na kuepukana na janga la njaa.
Mhe. Mtondoo ameyasema hayo alipokuwa kwenye kikao cha baraza la madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Agizo hili limetolewa kutokana mabadiliko ya hali ya hewa yaliyojitokeza kwa msimu huu, kwani Wilaya haikupata mvua za vuli za kutosha hivyo sehemu kubwa ya mazao yalikauka, aidha mbali na mvua za vuli, mvua za masika zimechelewa sana hali inayopelekea kutokuwa na uhakika wa mavuno kwa msimu huu.
“ Tukiendelea kuuza chakula nje ya Wilaya tunaamini tutakuwa na uhaba wa chakula ndani ya Wilaya yetu” alisema Mhe. Mtondoo alipokuwa akielezea hali ya chakula ndani ya Wilaya ya Kilindi.
Aidha Mhe. Mtondoo amewaasa wafanya biashara wa mazao kwendelea kuuza chakula ndani ya Wilaya ili kuweka uwiano wa chakula kwa maeneo ambayo hayakupata mavuno wakati wa vuli lakini pia wakulima kutunza akiba ya chakula waliyonayo.
Msimu uliopita wa mwaka 2018 Wilaya ya Kilindi ilipata jumla ya tani 62,020 za mahindi, tani 19,000 za maharage na tani 31,000 za muhugo. Hivyo Wilaya ilikuwa na ziada ya kutosha na kupelekea kuuza mazao hayo Wilaya na mikoa mbalimbali hata nchi za jirani.
Hata hivyo Wilaya ya Kilindi ni ya imeendelea kuongoza Mkoa wa Tanga kwa kuwasaidia wakulima wake kupata mkopo wa matrekta kutoka Serikalini kupitia shirika la NDC (National Development Cooperation), linalotoa mkopo wa Matrekta kwa wakulima kwa masharti nafuu, ambapo mpaka sasa wakulima kumi na tatu wa Wilaya ya Kilindi wamepata matrekta hayo.
Akizungumzia mkopo huo wa matrekta Mkurugenzi mtendaji Ndg. Gracian M.Makota amesema “ Mkoa wa Tanga umepokea jumla ya Matrekta kumi na tano na kati ya hayo kumi na tatu yameletwa Kilindi”.
Aidha Ndg. Makota amewataka waheshimia madiwani kuendelea kutoa elimu ya upatikanaji matrekata hayo kwa wakulima walio katika maeneo yao waweze kuboresha uzalishaji wa mazao lakini pia kuinua uchumi wao.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mussa Semdoe alitumia kikao hicho kuwapongeza watalaam wa Halmashauri na uongozi wa Halmashauri kwa kupata Hati safi kwa miaka Mitatu mfululizo.
Mwisho.
Imeandaliwa na:
Samweli D.Mwantona ( Afisa TEHAMA)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Ndg. Gracian Makota akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika leo tarehe 08.05.2019 katika ukumbi wa Halmashauri.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Mhe. Mussa Semdoe akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika tarehe 08.05.2019 katika ukumbi wa Halmashauri.
Diwani wa kata ya Bokwa Mhe. Idrisa Mgaza ( mwenyekiti wa kamati ya Uchumi ) akijibu maswali yaliyoelekezwa kwa kamati yake wakati wa kuwasilisha taarifa za kamati kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri siku ya tarehe 08.05.2019.
Baadhi ya waheshimiwa Madiwani walioshiriki kikao cha baraza la madiwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri siku ya tarehe 08.05.2019.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kikao cha baraza la madiwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri siku ya tarehe 08.05.2019.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.