Na Modi Mngumi-Songe
Jumla ya watu 77,567 wilayani Kilindi wamepima virusi vya Ukimwi katika kipindi cha Januari hadi Oktoba,2018.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa wilaya Kilindi Mh: Sauda Mtondoo katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani mwaka 2018 yaliyoadhimishwa kiwilaya katika viwanja vya stendi ya mabasi mjini Songe
Mh:Mkuu wa wilaya alisema kati ya watu hao waliopima, wanaume ni 29,950 na wanawake ni 47,617 na waliogundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni 801 ambapo kati yao wanaume ni 251 na wanawake ni 550.
Alisema kutokana na takwimu hizo, kiwango cha maambukizi ni sawa na asilimia 1.03 ikimaanisha kuwa katika kila watu 100 mmoja ana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
“Takwimu hizi siyo nzuri katika wilaya yetu bado tunalo jukumu kubwa la kuendelea kuhamasishana ili kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya VVU” Alisema Mh:Mtondoo na kuongeza kuwa mtizamo wa kitaifa,kimataifa kwa sasa ni kutokomeza maambukizi mapya ya VVU,Unyanyapaa na vifo vinavyotokana na Ukimwi.
Mh:Mkuu wa wilaya alisema ili kufikia lengo hili ni lazima kubadili tabia kwa kuvunja mtandao wa ngono zisizo salama na kuacha mila na desturi hatarishi kama ukeketaji kwa wanawake,kurithi wajane na ndoa za utotoni.
Alisema vijana na wanafunzi wapatiwe stadi za maisha zitakazowezesha kuchelewa kuanza kujamiiana,kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za unyanyapaa na ubaguzi kwa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI na kuwataka watoa huduma za Afya kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilindi bwana Gracian Makota akizungumza katika maadhimisho hayo aliwapongeza waliojitokeza katika kuchangia damu kwani itasaidia kuokoa maisha ya wananchi wengine watakaokuwa na uhitaji wa damu katika hospitali na kuwataka watu wengi kujitokeza kupima na kutoa damu.
Alisema vijana wapo kundi kufuatwa na watu wasio waaminifu na hivyo kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi,hivyo kulitaka kundi hili kuwa makini kuhakikisha hakuna mtu anaeweza kuharibu maisha yao na mipango yao ya baadaye.
Akizungumzia kuhusu waliogundulika kuwa na maambukizi ya VVU bwana Makota alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa dawa bure na watu hao kuweza kuishi maisha mazuri na marefu kama watu wengine ambao siyo waathirika.
Awali akisoma risala ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi mwaka 2018 ,Mratibu wa ukimwi wilaya Kilindi Dk Michael Chabai alisema Tangu wilaya ilipoanza kutoa matibabu kwa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi mwaka 2007 hadi Septemba 2018,jumla ya wateja 2,489 kati yao wanaume 773 na wanawake 1,756 wameandikishwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma wilayani hapa.
Alisema miongoni mwa wateja hawa ,1,315 wanapata dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi na kati yao wanaume ni 394 na wanawake ni 921.
Maadhimisho haya yalihusisha utoaji damu kupitia mpango wa damu salama,ujumbe kuhusu athari za ukimwi kutoka kwa vijana wa shule ya sekondari Seuta,utoaji huduma za uzazi wa mpango na upimaji wa Virusi vya Ukimwi.
Kauli mbiu ya Siku ya Ukimwi Kitaifa mwaka 2018 ni “PIMA,JITAMBUE,ISHI”
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.