Waratibu Elimu kata wilaya ya Kilindi wametakiwa kutozitumia pikipiki walizokabidhiwa kwa matumizi yao binafsi badala yake wazitumie katika matumizi ya ofisi tu, ilikuinua kiwango cha Elimu ndani ya Wilaya ya Kilindi.
Hayo yamesemwa leo katika kata ya Bokwa (eneo la Halmashauri) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Ndg. Clemence A.Mwakasendo alipokuwa akikabidhi pikipiki 21 kwa waratibu Elimu kata wilaya ya kilindi. Pikipiki hizo zimetolewa kwa ufadhili wa LANES (Literacy And Numeracy Education Support) kwa kushirikiana na Serikari.
Mwakasendo alisema dhamira ya Serikari ni kuinua kiwango cha Elimu hivyo amewataka Waratibu Elimu kata kutumia vifaa hivyo kwa kufuata taratibu lakini pia ameagiza kuhakikisha wanatoa taarifa ya matumizi ya pikipiki hizo kila robo mwaka na kufanyiwa ukaguzi.
“ Msizitumie pikipiki hizi kubebea mizigo na matumizi binafsi, maana sitoweza kuvumilia kuona zikitumika nje ya malengo yaliyokusudiwa lakini pia tofauti na maelekezo mtakayo pewa hii leo” Alisema Mwakasendo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Ndg. Clemence A.Mwakasendo (aliyevaa shati la mistari katikati) akiwaeleza jambo Waratibu Elimu Kata waliosimama kwenye pikipiki alipokuwa akiwakabidhi pikipiki hizo eneo la Halmashauri ya Wilaya siku ya Tarehe 06 Aug 2018. Kushoto kwake ni Afisa Elimu Msingi Ndg. Godfrey Abayo na Kulia kwake ni Afisa Utumishi Ndg. Edward Masona. Pikipiki hizo zimetolewa kwa ufadhili wa LANES (Literacy And Numeracy Education Support) kwa kushirikiana na Serikari. Picha na Ndg Samwel D.Mwantona ( Afisa TEHAMA ).
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji aliahidi kushirikiana na Jeshi la polisi ilikuhakikisha Waratibu wasio kuwa na Leseni za udereva wanaandaliwa utaratibu maalumu wakuzipata ikiwa ni pamoja na mafunzo ya udereva ili kutokuvunja sheria na taratibu za barabarani.
Nae Afisa Elimu Msingi Ndg. Godfrey Abayo aliishukuru Serikari kwa msaada huo na kuwaasa waratibu kufanya kazi kwani changamoto ya usafiri iliyoonekana kuwa kubwa kulingana na jiografia ya maeneo ya wilaya ya Kilindi sasa Serikari imeitatua.
Hata hivyo Afisa Elimu Sekondari Bi. Mkenda aliwaasa Waratibu kuzitunza pikipiki hizo ili hata wao watakapoondoka wazikabidhi kwa wenzao zikiwa katika ubora mzuri kwani ni kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo pia amewaasa kuwa makini na namna ya kuzihifadhi kwani kuna wezi wanaozihitaji lakini pia watu walio na niambaya na Serikali.
Mwenyekiti wa Waratibu Elimu kata Ndg Eliewaa Magata kwa niaba ya wenzake aliwea kutoa shukrani kwa Serikari na Wafadhili kwa kuweza kuona Changamoto kubwa wanayokabiliana nayo katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kwa Wilaya ya Kilindi kulingana na maeneo yake, hivyo ameomba Serikali kuendelea kutazama sekta HIi ya Elimu ili kuweza kuutokomeza ujinga kwa kizazi hiki na kijacho lakini pia ameeahidi kusimamia maelekezo yaliyotolewa katika matumizi ya pikipiki hizi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Ndg. Clemence A.Mwakasendo ( Aliyepanda pikipiki ) alipokuwa akiendesha moja ya pikipiki ikiwa ishara ya uzinduzi wa pikipiki hizo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, siku ya tarehe 06 Aug 2018. Wengine katika picha ni wakuu wa Idara mbalimbali pamoja na Waratibu waliokuwa wakishuhudia tukio hilo. Pikipiki hizo zimetolewa kwa ufadhili wa LANES (Literacy And Numeracy Education Support) kwa kushirikiana na Serikari. Picha na Ndg Samwel D.Mwantona ( Afisa TEHAMA ).
Wafadhili Literacy And Numeracy Education Support (LANES) kwa kushirikiana na Serikari wametoa pia Komputa tatu za mezani, Meza tatu, Viti vitatu na “printer” moja kwa matumizi ya idara ya Elimu Msingi na Sekondari kwa Halmashauri ya Wilaya ya KIlindi.
Aidha ni wakati umefika wa kuiunga mkono Serikali kwa juhudi inazozionyesha hasa katika sekta hii ya Elimu, kwani nasisi kama wadau tunanafasi yetu katika sekta hii. Serikali imetoa elimu bure kwanzia shule za Msingi hadi kidato cha nne hali iliyopelekea ongezeko kubwa la wanafunzi shule la msingi, lakini pia imegawa vitendea kazi kama vile vitabu katika shule mbalimbali.
Je! Wewe kama mdau wa Elimu umefanya nini katika Sekta hii ya Elimu ? pili unadhani kizazi kijacho kitakumbuka mchango gani ulioutoa katika Sekta hii? Mwisho ni njema ukatambua urithi uliobora kwa mototo ni Elimu hivyo ni busara ukaiunga mkono Serikali katika juhudi za kuboresha na kuinua kiwango cha Elimu Tanzania.
Copyright ©2018 Kilindi DC . All rights reserved.